Mafanikio

Anza Mwaka Mpya Kwa Vitendo na Sio Mipango Pekee na Ndoto

anza-mwaka-mpya-kwa-vitendo-1

Ili uweze kufanikisha malengo yako ya mwaka ni muhimu sana kuanza mwaka mpya kwa vitendo zaidi. Mipango pekee bila vitendo ni sawa na ndoto za mchana. Sababu mojawapo kubwa ya mipango mingi kushindwa ni “Mipango bila Vitendo”. Kuna sababu nyingine zinazochangia kushindwa kwa malengo mengi kila mwaka lakini hii ni kubwa na ni muhimu tukaiangalia hapa.

Ili kufanikiwa katika kila lengo la binadamu ni muhimu sana kuweka mikakakati ya vitendo. Nini kitafanyika kwenye kila lengo ili kufikia mafanikio.

Mikakati hii ni lazima iwe halisia,inayowezekana kufanyika na yenye muda maalumu mfano kilasiku,kilawiki au katika kipindi fulani mfano mwezi mmoja au miezi sita.

Mipango Pekee Haileti Matokeo bali Vitendo

anza-mwaka-mpya-kwa-vitendo-2

Mojawapo ya tabia moja ambayo inawafanya Wenye Mafanikio kushinda na Wasiofanikiwa kushindwa ni tabiaya KUANZA kufanya jambo.

Nidhamu ya kuanza kufanya jambo kama ulivyopanga ni kigezo kimoja kikubwa kupelekea katika mafanikio.

Hivyo katika malengo yako ya mwaka mpya au wakati mwingine wowote,thubutu kuanza kutekeleza hatua ya kwanza.

Katika safari ya kilometa 100 sirahisi kuona mwishoni,bali unaweza kuona mwanzoni na hatua kadhaa mbele. Chukua hatua ya kwanza na kila unavyoenda mbele utaona njia ikifunguka na hatimaye utafika mwisho wa safari.

Weka Muda wa Kuanza Kuwa Karibu

Kwa hiyo kwenye kila lengo lako la mwaka andika vitendo utakavyofanya na anza mara moja. Weka muda wa kuanza karibu inavyowezekana. Kama unaanza januari,basi sema januari 2 . Akili inafanya kazi zaidi kwa jambo lililo karibu kuliko lililo mbali.

Fuatilia Maendeleo ya Kila Kitendo

Kila kitendo katika utekelezaji wa malengo kitawekewa muda wa kuanza na kuishia,untakiwa kufuatilia matokeo ya utendaji kwenye kila kituo. Hakiki kama umetenda kama ulivyopanga.

Kwa kufanya hivi utahakikisha unaenda sawa kuelekea kufikia lengo lako

Kubadilisha Mbinu za Kufikia Lengo

Jihakiki kuona kama unaendelea vizuri kufikia lengo kila baada ya muda fulani. Nashauri kila baada ya miezi mitatu. Kama unafikiri mbinu unazotumia haziendi vizuri basi unaweza ukaongeza nyingine au kubadirisha zile za awali ili kuharakisha utekelezaji.

Kutofanya uhakiki katikati ya safari kunafanya watu wengi kutoka nje ya njia na kujikuta hawafiki pale walipotarajia.

Weka Malengo Machache Tu Yanayowezekana

Sababu nyingine kubwa ya kushindwa kufikia malengo kwa wengi ni kumega mkate mkubwa kuliko uwezo wa kutafuna. Tunapanga mengi sana katika muda mfupi na katika uwezo mdogo. Malengo yako lazima yawe halisia na yanayowezekana kutegemea na uwezo wako wa kiafya,kiakili na kifedha.

Panga mambo machache yanayowezekana na ambayo yanataleta mabadiliko makubwa.

Kumbuka Sheria ya 80-20 inayosema Asilimia 20 tu ya mambo utakayofanya yataleta asilimia 80 ya matokeo yako. Chagua mambo machache muhimu yatakayoleta mabadiliko katika maisha yako katika kipindi husika.

Jenga Tabia ya Kuchukua Hatua na Sio Kulalamika

Kila mtu anatengeneza ulimwengu wake mwenyewe kwa kumaanisha kuwa mazingira na hali uliyonayo inajengewa na wewe mwenyewe. Mabadiliko yako mikononi mwako,kama huipendi hali fulani basi chukua hatua ya kuibadilisha hali hiyo. Kuwa chachu ya mabadiliko yako na jamii yako.

Watu wengi wamekuwa na kasumba ya kulalamikia kila jambo, utasikia “Serikali haijengi barabara” au “Walimu hawafundishi mashuleni” lakini jiulize wewe umefanya nini klubadili hali hii.

Umewahi kumtafuta mbunge wako na kujadili naye suala hili au mwenyekiti wa mtaa wako au hata majirani zako kuhusu kuchangia kuvu zao katika kuboresha miundombinu katika eneo lako tu angalau?

Je umewahi kwenda shuleni kwa watoto wako ukaongea na mwalimu mkuu au mwalimu wa taaluma kuhusu elimu duni inayotolewa?

Hebu tujenge utamaduni wa kuchukua hatua ili kubadili mambo.

Tabia hii ni muhimu sana pia katika kufikia malengo yako binafsi ya familia na kazini kwako,kama umekuwa kimya juu ya mambo yanayokutatiza basi anza sasa kama mojawapo ya lengo lako la mwaka mpya.

Anza Mwaka Mpya Kwa Malengo yenye Vitendo

anza-mwaka-mpya-kwa-vitendo-3

Maisha yako yatakuwa tofauti sana ukiwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno na hivyo ndivyo itakavyokuwa mwishonimwa mwaka huu kama utabadili tabia na kuwa mtendaji na mtu anayechukua hatua kwanza katika kila jambo.

Mipango pekee bila vitendo ni sawa na ndoto. Utaamka mwishoni mwa mwaka na hakuna hata moja ambalo ulipanga litakalokuwa limefanikiwa. Anza mwaka mpya kwa vitendo na siyo mipango pekee.

Andika malengo yako na weka vitendo kwenye kila lengo. Kumbuka ni LAZIMA uandike kwani “Kisicho andikwa hakipo “. Akili yako inafanya kazi zaidi kwa yale mambo yaliyoandikwa na ambayo kila siku utarudia kuyasoma na kutenda.

Nakutakieni heri ya mwaka mpya na mipango yenye malengo na vitendo.

 

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment