Familia Jamii Utamaduni

Changamoto za Kulea Watoto wa “Dijitali” kwa Wazazi wa “Analojia”

kulea-watoto-wa-digitali-1

Tabia ya mtu inatokana na malezi aliyoyapata kwa kiasi kikubwa toka kwa wazazi,pia toka kwa walimu mashuleni, mafundisho ya dini,na toka kwa watu anaoonana nao na kuchangamana nao kila siku za maisha yake hasa wakati wa umri mdogo. Kulea watoto kulingana na tamaduni zetu katika karne hii ya teknolojia ni changamoto kubwa.

Watoto wa Dijitali ni wale ambao wamezaliwa katika karne hii ambayo teknolojia ya habari na mawasiliano imesomnga mbele sana kiasi ambacho taarifa zimekuwa nyingi kupita uwezo wakuzidadavua. Wazungu wanaita “Information Overload“.

Watoto hawa wa dijitali wanafahamu mambo mengi sana kuliko ambavyo wanatakiwa kufahamu katika umri husika jambo ambalo linaleta changamoto kubwa katika kulea watoto kwa wazazi wa zamani ambao walizaliwa kipindi ambapo teknolojia haikuwa katika kiwango hiki na mfumo wa malezi walioupata unatofautiana sana na wa sasa na pengine haufanyi kazi katika mazingira ya kisasa. Wazazi hawa nimewaita “Wazazi wa Analojia”.

Katika hali hii utakuta mtoto anafahamu mambo mengi tu ambayo wazazi hawayajui,ina maana mzazi anajifunza toka kwa mtoto,hii ina maana gani? Kuna madhara mara mbili

  1. Mzazi anakosa kujiamini katika jukumu lake la kumfundisha mtoto kwani anatambua sasa kuwa mtoto ni mjuaji wakati ungine kumzidi,na anaweza kuamua kutofanya hilo jukumu kwa kujua mtoto anafahamu tayari. Wakati mwingine inakuwa si sahihi.
  2. Mtoto anatambua baada ya muda kuwa mzazi wake hafahamu mambo mengi na kuwa yeye anafahamu zaidi. Hivyo naye anaacha kuuliza au kutaka kufahamu toka kwa wazazi. Hivyo anaweza akafanya vitu kwa ufahamu wake tu binafsi au kwa kutafuta msaada sehemu nyingine nje na wazazi wake. Na huenda msaada atakao pata ukawa sio sahihi.

Hali hii ni hatari katika ulezi wa watoto katika jamii yetu na ni lazima kuliangalia kwa mapana sana na kuchukua hatua stahiki.

 

Vyanzo Vikubwa vya Habari kwa Watoto

Kuna vyanzo vingi vya taarifa kwa watoto nyingi hazina chujio la umri kama falsafa za malezi zinavyoelekeza. Na hapa tuviangalie vitatu vikubwa:

# 1. Televisheni (TV) na Video

kulea-watoto-wa-digitali-TV-1

Ni kitu cha kushangaza kuwa miaka 20 tu iliyopita hakukuwa na TV katika nchi hii ukiachia ile ya Zanzibari (TVZ). Lakini sasa hivi kuna utitiri wa TV kila mahali nchini. Nyingine ni za ndani na nyingine ni toka nje.

Vipindi vya TV vinatofautiana na vinatoa habari mbalimbali. Nyingine ni nzuri kwa watoto na nyingine si nzuri sana. Mfano kuna baadhi ya TV za nje ambazo zinaonyesha vipindi vya ngono usiku kwa kutegemea watoto wamelala. Lakini watoto wakijua kuna vipindi hivi huenda wakaamka usiku wazazi wakiwa wamelala na wakaziona. Lakini usiku kwa nchi moja inaweza ikawa mchana kwa nchi nyingine,hivyo hiyo ni changamoto katika kulea watoto wetu.

Sia ajabu pia ukakuta TV chumbani kwa watoto siku hizi,hii inaongeza hatari iliyopo katika kuchuja taarifa toka katika TV.

Sinema na tamthilia zimekuwa mojawapo ya vipindi katika TV ambazo wengi wakiwemo watoto wanapenda kuziangalia. Japo vipindi na sinema hizi zinaweka kiwango cha chini cha umri wa waangaliaji,lakini ni ngumu kwa wazazi kusimamia hilo. Hivyo watoto wengi wanapata habari na mafunzo yasiyofaa kwa jamii zetu. Aidha yanakiuka mila,desturi na utamaduni wajamii wanazoishi au zinafundisha mambo ya kikatili kama vile vipindi vya mieleka na sinema na mauaji ambazo zinawajenga watoto katika misingi isiyofaa, kwani kwa watoto hiyo ni halisia na sio maigizo.

# 2. Simu za Mikononi

kulea-watoto-wa-digitali-3

Matumizi ya simu za mikononi yameleta mapinduzi makubwa katika jamii zetu kwa kuboresha mawasiliano. Kusambaa kwake kila sehemu nchini hata vijijini kumewezesha mawasiliano ya kibiashara na kijamii kuwa rahisi na kupunguza gharama kwa wengi.

Lakini pia kumeleta mpasuko mkubwa wa kimaadili si kwa watoto peke yake bali hata kwa wazazi wenyewe.

Wizi , udanganyifu kati ya wapenzi ni mojawapo tu ya mifano ya matumizi mabaya ya simu.

Siku hizi inakuwa kitu kinachozoeleka kwa watoto kuwa na simu,hata wakiwa shuleni. Kwa maelezo kuwa wazazi wangependa kuwasiliana na watoto wao wakiwa mbali. Ni kweli,hiki ni kitu kizuri lakini kinacholeta shida ni matumizi mabaya ya simu hizi. Mtoto akiwa na simu ataanza kuwasiliana na watu tofauti na si wote kati ya hao ni watu wema.

Kwa watoto wa kike hii ni hatari kubwa zaidi,kwani simu hizi huenda zikatumika kupanga mipango na wanaume wasio na malengo mema nao na mwishowe wakaingia katika ngono na mimba za utotoni.

Shida nyingine ya simu kwa watoto ni kasumba ya matumizi,simu zinaweza zikawafanya watoto kutokuwa makini na kutozingatia sana masomo yao. Kwani watatumia muda mwingi kuchati na marafiki na kucheza michezo iliyomo katika simu hizi.

# 3. Intaneti na Mitandao ya Kijamii

kulea-watoto-wa-digitali-intaneti-1

Mtandao wa intaneti umekuwa chanzo cha taarifa nyingi duniani kote,mapinduzi ya simu yamechochea upatikanaji wa mtandao huu. Mwanzoni ilikuwa ni lazima uwe na kompyuta,na kompyuta zilikuwa si kwa kila mtu sababu ya gharama kuwa kubwa. Sasa hivi mambo ni tofauti,kompyuta ziko karibu katika familia na watu binafsi. Intaneti nayo ni rahisi kupatikana kwa kupitia simu kwenda kompyuta au modemu.

Hii imerahisisha sana mawasiliano na upatikanaji wa habari mbali mbali toka katika mtandao huu. Habari zilizomo katika mtandao wa intaneti hazichujwi kwa kuangalia rika la watumiaji. Humu unaweza ukapata habari nzuri za kuelimisha hali kadharika habari za kupotosha. Kwa namna hii watoto wanaomiliki simu au kompyuta zenye kuunganishwa katika mtandao wa intaneti wanaingia katika hatari.

Pia Mitandao ya kijamii kama facebook na twitter ni maarufu sana na inatumiwa na watoto pia na ndani yake kuna mambo mengi, mazuri na mabaya kwa watoto.

Udhibiti wa Matumizi ya Vyombo Vya Habari kwa Watoto Unahitajika

Serikali iweke mwongozo juu ya udhibiti wa habari zinazowafikia watoto. Zitungwe sheria zitakazodhibiti suala hili ili kusaidia wazazi kulea watoto katika maadili yanayostahili.

Walezi pia wanaweza kuchukua hatua kadhaa za kuongeza udhibiti

# 1. Udhibiti kwenyeVipindi vya Televisheni na Video:

Wazazi na walezi wanaweza wakaweka udhibiti nyumbani kwa kufanya yafuatayo:

  1. Kutoweka TV vyumbani kwa watoto
  2. Kufunga chaneli zisizofaa kwa kuweka neno siri
  3. Kuzui sinema zisizohitajika kwa watoto majumbani

# 2. Udhibiti wa Matumizi ya Simu:

Wazazi na Walimu mashuleni wanaweza wakaweka mikakati juu ya udhibiti wa matumizi mabaya ya simu mashuleni kwa kuzuia kabisa umiliki wa simu kwa watoto.

Mawasiliano kati ya wazazi na walimu yapitie kwa simu ya shuleni au walimu pekee.

Kwa watoto wanaoishi na wazazi wao,simu si muhimu sana kwao pia hivyo zinaweza zikazuiwa. Lakini kama zi lazima mtoto awe na simu basi wazazi wazifuatilie kujua nani anapiga na kupigiwa na ujumbe unaotumwa kwa kuzipitia simu moja kwa moja au kutumia programu maalumu katika simu zitakazo tuma ujumbe kwa mzazi au kwa kupata taarifa toka makampuni yanayotoa huduma za simu.

# 3. Udhibiti wa Intaneti na Mitandao ya Kijamii

Wazazi wanaweza wakatumia programu katika simu kufunga baadhi ya taarifa au tovuti zisizohitajika kwa watoto. Watoa huduma wam intaneti wanaweza wakafanya hivyo pia kufunga taarifa ambazo hazihitajiki kartika simu ya mtoto.

 

Juhudi za pamoja kati ya Serikali,Wazazi na Walezi Zinahitajika Kudhibiti Hali

Kama taifa kwa ujumla,wazazi na walezi wa watoto wakichukua hatua za pamoja,tutajenga taifa ambalo watoto wanapata kile wanachokihitaji katika malezi katika wakati muafaka. Hii itawarahisishia wazazi na walezi kuwakuza watoto katika maadili sahihi ya jamii zetu.

Ili kukabiliana na watoto wa dijitali ni lazima wazazi nao wahame toka analojia kwenda dijitali vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi kadili utofauti wa ufahamu wa teknolojia unapokuwa mkubwa kati ya watoto na wazazi.

Kama wewe ni mzazi au mlezi,tupe uzoefu wako juu ya suala hili. Unakabiliana vipi na tatizo hili? Tuandikie katika kisanduku cha majibu hapo chini.

 

&nbsp

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment