Utamaduni

Kutowajibika,Uzembe,Rushwa na Ufisadi: Je ni Utamaduni wa Watanzania?

uzembe-rushwa-na-ufisadi-4

Nchi nyingi za Afrika zilipopata uhuru wake katika miaka ya 60 zilikuwa na malengo ya kujenga uwezo wa kujitegemea kwa viongozi wazelendo na kwa wananchi wake kwa ujumla. Kujenga taifa jipya lililo huru lenye kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yake yenyewe na sio kutegemea misaada toka nje.

Tanzania (Wakati huo ikiwa Tanganyika na Zanzibar) ilikuwa miongoni mwa nchi hizi. Chini ya uongozi mahiri wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika kulikuwa na mikakati ya kufanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo yenyewe. Kulikuwa na kauli mbiu kama “Uhuru ni Kazi” ambao lengo lake lilikuwa kuwapa ari wananchi wa Tanganyika kufanya kazi kwa bidii ili kuwa na uhuru wa kweli.

Nchi yenye maendeleo ni lazima ijengwe na wananchi wenye kufanya kazi kwa bidii,wenye kujituma na wanaowajibika katika majukumu yao.

Wananchi wazalendo ambao siku zote wako mstari wa mbele kuijenga ,kuilinda na kuitetea nchi yao. Wale ambao wanaweka maslahi ya taifa mbele kwanza dhidi ya maslahi yao binafsi.

Haya yote ni historia katika nchi yetu,tunayasoma kwenye vitabu tu na kinachofanyika sasa hivi ni kinyume kabisa.

Uzembe na Uvivu wa Kazi Umekithiri

Imesemwa kuwa mazoea hujenga tabia na tabia hujenda desturi. Desturi ni msingi mkubwa wa utamaduni katika jamii husika,hii ina maana kuwa tabia ya uzembe na uvivu kazini inajenga desturi kwa watanzania na hivyo kuwa utamaduni-Mfumo wetu wa maisha.

Watanzania ni wavivu sana katika ufanyaji kazi. Asilimia zaidi ya 60 katika nchi hii ni tegemezi katika hao asilimia 48 ni watoto na wazee(miaka 0-14,64+) lakini kama asilimia 20 ni watu wenye nguvu za kufanya kazi na hawafanyi kazi.

Wengine wanasingizia kuwa hakuna ajira,kama nilivyosema kuwa hiki ni kisingizio kwa sababu kuna vitu vingi tu ambavyo mtu anaweza kufanya katika nchi hii nje ya ajira toka katika makampuni na mashirika ya umma ambayzo zinaweza kuwaingizia kipato.

Kilimo, Biashara na Ufugaji ni baadhi ya sehemu ambazo zinatoa fursa kubwa tu ya kujiajiri.

Lakini ukiachia hawa wasiofanya kazi ,hata wale ambao wako kazini uzalishaji wao ni mdogo sana. Katika masaa 40 ambayo mfanyakazi kwa kawaida anatakiwa kufanya kazi walio wengi wanafanya nusu tu ya muda huo. Masaa mengine atakuwa anayatumia kufanya mambo ambayo si malengo ya ajira yake.

Mfano: Kama alitakiwa kuingia ofisini saa 2 asubuhi ataingia ofisini saa moja baadae,akija atafanya kazi saa moja (Saa 3-4) kisha ataenda kunywa chai ambako atatumia kama dakika 30 labda, Saa 4:30 atafanya kazi mpaka saa 6:30 ambapo ataenda kula chakula kwa saa moja mpaka moja na nusu. Saa 8:00 mchana atarudi kufanya kazi mpaka saa 10.00 jioni atarudi nyumbani. Jumla ya masaa aliyotumia nje ya nuda wa kazi ni matatu(3). Hivyo ametumia masaa 5 katika 8 kufanya kazi.

Na katika kufanya kazi yenyewe bado utaona mtu mmoja anatoka kwenye kiti chake na kwenda kwa mwingine na kufanya maongezi yasiyohusu kazi. Mabishano juu ya timu za mpira wanazozipenda na majungu ni mojawapo ya vitu vingine vinavyopunguza muda wa kazi sehemu za kazi.

Hili ni balaa kubwa na linaathiri sana uzalishaji. Napenda kujisemea binafsi kuwa kama ningepata nafasi ya kuwa raisi wa nchi hii kitu kimoja na kimoja tu ambacho ningefanya ili kufanya nchi hii ijitegemee ni kuhakikisha watu wote wenye uwezo wa kufanya kazi wanafanya kazi.

Hii peke yake inaweza kuifanya nchi hii ijitegemee na isiombe misaada kwa ajili ya kukidhi bajeti ya nchi.

Wageni wanachukua kazi zetu
Kwa uvivu huu, wawekezaji toka nje wanapata wakati mgumu kuwapa watanzania kazi. Makampuni mengi hayawaweki watanzania katika nafasi nyeti. Mameneja wengi si wazawa wa Tanzania. Watanzania wanafanya kazi za punda tu,na tutaendelea kufanya hivyo mpaka mabadiliko yafanyike.

Binafsi nikiwa katika nafasi ya kuchagua kuwa nani apewe kazi ambayo ataifanya kazi kwa ufanisi na kwa wakati na kujituma nitapata wakati mgumu kumchagua Mtanzania. Sitaweza kuwa na vigezo vya kujiridhisha kwa nini nimchague mtanzania labda tu kwa kuwa ni mtaifa mwenzangu;na hili ndilo kubwa linalotuponza katika hii nchi.

Kufanya Kazi Masaa ya Ziada Kwa Maendeleo Binafsi
Watazania walio wengi hawawezi kuongeza hata saa moja tu ya kazi ili kumalizia jambo muhimu.Tunaongozwa zaidi na muda na sio ukamilifu wa kazi yenyewe. Tuna kaa ofisini tukiangalia saa. Zikibaki dakika 10 utaona watu wanaanza kukukusanya mabegi na mikoba tayari kuondoka.

Mwalimu wangu mmoja wa maendeleo binafsi (Brian Tracy) anasema “masaa 8 ni kwa ajili ya kula na masaa ya ziada ni kwajili ya maendeleo yako binafsi” Yaani ili ufanikiwe ni lazima uende hatua moja zaidi ya pale ulipopangiwa.

Wizi,Rushwa na Ufisadi imekuwa Desturi ya Watanzania

Viongozi wetu wamekuwa walafi, wanataka kula zaidi ya kile wanachostahili na walichofanyia kazi. Maslahi yao yako mbele kuliko ya jamii wanayoingoza. Ubinafsi umekithiri kiasi ambacho hakuna anayeangalia maslahi ya nchi.

Kiongozi mwenye dhamana anasaini mkataba usio na manufaa kwa watu wake kwa sababu tu ameahidiwa asilimia fulani ya fedha itakayotolewa bila kujali madhara ya wananchi walio wengi.

Kila mtu leo anakimbilia kwenye siasa,kwani huko ndiko kuna nafasi ya kupakua zaidi kuliko sehemu nyingine. Tumeshuhudia wasomi na wataalamu wa fani mbalimbali akikimbilia kwenye siasa. Siasa imeonekana kuwa njia ya mkato kwajili ya mafanikio ya haraka haraka.

Wahoji leo viongozi wetu kujua nini kinawafanya wawe viongozi au watake kuwa viongozi?-Jibu ni mafanikio binafsi na ya mkato.

Fedha zinatumika kutoa rushwa ili kununua uongozi na viongozi hao wakiingia madarakani wanafuja mali ya umma kwa mslahi yao binafsi (Ufisadi).

Zamani ilikuwa ukimuuliza mtoto ukiwa mkubwa unataka uwe nani alikuwa anasema “nataka kuwa daktari” au “nataka kuwa mwalimu”. Leo hii ukiuliza hivyo utajibiwa “nataka kuwa waziri au mbunge”.

Wafanyakazi wakistaafu katika makampuni wanakimbilia kwenye siasa. Kama wamestaafu kwa kuwa wamezeeka na wamechoka inakuwaje waweze siasa? Siasa ni rahisi hivyo siyo? Mimi sina majibu ya haya.

Mapendekezo Juu ya Kubadili Hali Hii ya Hatari Kwa Taifa

Ni lazima tuchukue hatua,na tubadilike na haya ni bbadhi ya mapendekezo ya mabo ya kufanya ili tuongokane na utamaduni huu mbaya ambao unaendelea kukua:

 1. Tuchague viongozi wachapa kazi na wawajibikaji
  Wananchi tuchague viongozi wenye kuwajibika. Viongozi wazalendo na ambao wako tayari kuleta mabadiliko ya kweli. Wahamasishe utendaji kazi na kuwajenga vijana toka shule za awali mpaka vyuo vikuu.
 2. Elimu ya Uraia Mashuleni na Vyuoni
  Elimu ya uraia iongezewe chachu na ifundishe uzalendo kwa nchi yao.
 3. Sheria Kali Dhidi ya Mafisadi
  Sheria kali zitungwe dhidi ya mafisadi, wabadhilifu wa mali za umma na wala rushwa zitungwe na kusimamiwa. Viongozi wabadhilifu wanyang’anywe madaraka, wafilisiwe na kushitakiwa.Tabia ya kulindanana kuoneana aibu ikomeshwe.
 4. Sheria Kali Dhidi ya Wavivu na Wazembe:
  Sheria zitungwe kwa ajili ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini hawafanyi kazi wa kujishughulisha kwa lolote. Wakati wa kazi watu wote na wafanye kazi.
 5. Elimu ya Ujasiriamali kwa Wananchi
  Kuwekwe mikakati ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi ili kupunguza utegemezi. Lakini pia ili kuondoa visingizio vya kukaa bila kazi.
 6. Kuwekwe Mikopo ya Biashara
  Mikopo kwaajili ya biashara itolewe kwa masharti nafuu kwa wanachi wenye mipango ya biashara.
 7. Kuondoa Mfumo wa Ajira za Kudumu Serikalini:
  Serikali iondoe ajira za kudumu kwa wafanyakazi wake. Kwani hii ni sababu kubwa kwa wafanyakazi wake kutowajibika.Badala yake wafanyakazi wajiriwe kwa mikataba ya muda mfupi ambayo inaweza kuongezwa kutokana na utendaji wao katika mkataba wa nyuma.Pia mfumo wa upimaji utendaji kazi uongezewe nguvu na matokeo yake yafanyiwe kazi katika kupandisha vyeo au kushushwa.

Je Uvivu,Uzembe,Rushwa na Ufisadi ni Utamaduni wetu?
Ndiyo na hapana.

Ndiyo kwa sababu ni kweli imekuwa desturi yetu kufanya haya kama ambavyo tunajionea katika maisha yetu ya kila siku. Na ni lazima tuamue kwa pamoja kubadilika.

Hapana kwa sababu tukiangalia tulikotoka hatukuwa hivi. Tulikuwa na watu wawajibikaji na wazalendo. Tumebadilika taratibu na sasa tumefiia hapa. Kama inavyojulikana tabia,desturi na hata utamaduni hubadilika kama ambavyo imetokea,basi tunayo nafasi ya tubadilika tena kujenga utamaduni mzuri wa wananchi wawajibikaji,wazalendo,watendaji kazi na wanaochukia uzembe,rushwa na ufisadi.

Tupe maoni yako juu ya hili. Andika maoni katika kisanduku cha maoni chini ya

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment

2 Comments

  • Ili kutatua tatizo ni lazima kutambua tatizo kwanza na kisha kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
   Kila mmoja wetu na aanze yeye binafsi na eneo la mamlaka yake. Kama wewe ni baba wa familia basi anza toka nyumbani kwako,hakikisha watu wanajua wajibu wao na wanatekeleza.

   Sehemu yako ya kazi hali kadhalika,hakikisha wafanyakazi ndani ya kitengo chako wanawajibika na wewe mwenyewe uwe mfano. Tuache kuoneana haya.