Jamii Mafanikio

Mambo 8 Yanayomfanya Mtu Kupendwa na Watu

Kupendwa na Watu

Kila mtu anahitaji kupendwa kama mtu,mzazi,mwenza,mtoto au mfanyakazi. Inaleta raha na faraja kubwa moyoni. Lakini wakati mwingine si rahisi sana kupendwa na watu wengi. Wengine wanasema kuwa haiwezekani kupendwa na kila mtu,kwasababu kila mmoja ana vigezo tofauti vya kuchagua nani anampende na kinyume chake. Ila kuna vigezo ambavyo watu wengi wanathiriwa navyo juu ya maamuzi yao ya kupenda. Kwakweli maamuzi haya si ya hiyari ila yanakuja kwa hisia zaidi kutoka katika mawazo ya kina ambayo yanaongoza hisia za watu.

Hisia hizi zinajijenga taratibu ndani ya moyo wa mtu kutokana na matukio yanayotokea kila siku au kila mara na kuwekwa katika mawazo ya kina.

Ili upendwe na watu unatakiwa kujenga tabia amabazo watu watazipenda na hivyo wewe mwenyewe kupendwa. Kumbuka unatakiwa kujenga tabia na si kufanya kama roboti. Haya yanatakiwa kutoka ndani ya moyo wako. Unatakiwa kuwa halisi na sio kuigiza vinginevyo hutapata matokeo mazuri.

Pi Soma: Maneno 4 Rahisi Lakini Muhimu Mke Anahitaji Kusikia Kila Siku

Tabia 8 Kuu za Kupendwa na Watu

Kuna mambo mengi ambayo yanachangia kupendwa lakini haya ni yale ambayo nimeyaona yanamchango mkubwa na kama yakifanywa kwa ukamilifu yataweza kukupa matokeo mazuri na ukafanikiwa sana katika kuishi na kufanya kazi na watu sehemu yoyote iwe ni kazini nyumbani au sehemu nyingine za kijamii.

  1. Gusa nyoyo zao-Shiriki Hisia zao

Binadamu wanaongozwa na hisia zaidi,maamuzi mengi bado yanategemea hisia kuliko utashi.

Ingia katika nyoyo zao na ufahamu nini kimo ndani na uwe mshiriki.

Fahamu kuhusu afya zao kwa kwenda zaidi ya salamu ya kawaida. Uliza juu ya watu wanaowapenda sana na wanaomaanisha maisha yao kama watoto,wenza au wazazi.

Uliza maswali kama “Watoto wanaendeleaje? Wako darasa la ngapi?” ukiweza taja majina yao katika mazungumzo “John na Maria wanaendeleaje? Wameanza shule?”

Kama ni kazini ulizia kuhusu mradi wa mfanyakazi mwenza wako, “Umefikia wapi na mradi wako wa kutokomeza malaria?”

Shiriki katika mambo ya kijamii,sikukuu za kuzaliwa,misiba na sherehe kama harusi.

  1. Kuwa Msikivu

Katika mazungumzo,jenga tabia ya kusikiliza zaidi kuliko kuongea. Ongea pale mwingine anapokuwa amemaliza kusema. Usifanye kitu chochote kingine ukiwa unaongea na mtu kama vile kutuma ujumbe katika simu na muangalie usoni. Kwa namna hii unaonesha kujali anachosema na hukupandisha katika alama za kupendwa.

Kama uko katika nafasi za uongozi iwe nyumbani,kazini au sehemu nyingine,toa nafasi kwa watu kuongea na kutoa mawazo na hisia zao,kisha toa mtazamo wako au ushauri juu ya suala husika. Wakati unafanya hivyo usioneshe hata kidogo kuwa mawazo yao hayana maana. Sababu kila jambo lina maana,kama simkwako basi kwa aliyeliongea. Jali mawazo ya kila mtu.

  1. Kuwa Mkweli na Timiza Ahadi

Sema kweli mara zote,ukweli utalkuweka huru lakini kubwa zaidi watu watakupenda na watakuwa wakweli kwako pia.

Ahidi kilichopo ndani ya uwezo wako na utimize kwa wakati uliosema kuwa utafanya.

  1. Onesha Mfano,Tembea Katika Maneno Yako

Ongoza kwa mfano,fanya yale unayoamini na unayoyasema. Katika nafasi za uongozi ni vizuri kufanya japo kwa kiasi fulani kile unachowapangia wengine kufanya. Katika mazingira ya nyumbani unaweza ukaamua kulisha mifugo wikiendi mojaau kukata majani viungani.

  1. Toa Msaada

Saidia pale inapowezekana. Saidia wasiojiweza kama katika majumba ya kutunza wazee,walemavu au watoto wenye mazingira magumu.

Saidia ndugu na jamaa katika shida zao za msingi kama elimu au masula mengine ya kijamii kama misiba na magonjwa .

Saidia watoto katika masuala yao ya masomo,unaweza kuchagua somo moja kama kiiengereza au hesabu na kuwafundisha angalau kwa wiki.

Msaidie mweza wako katika kazi mbalimbali nyumbani. Kama wewe ni Baba basi msaidie mkeo kazi za nyumbani kama kufua kunyosha n.k kila inapowezekana.

  1. Toa Shukurani na Pongezi

Shukuru kwa kila jambo zuri hata kama likiwa dogo kwa namna gani. Sema “Asante” neno hili lina maajabu makubwa ambayo hatuyatumii inavyopaswa.

Kushukuru kunaonesha kujali juhudi za mwingine na zinafanya urahisi wa kupata tena siku nyingine au mara nyingine. Inasemwa kuwa kushukuru ni kuomba tena.

Kutoa pongezi ni namna nyingine ya kuvuta upendo toka kwa watu. Katika kila kizuri kinachofanya na mtu usisite kutoa pongezi. Unapopongeza huongeza nguvu na jitihada kwa mlengwa na kuweza kufanya bora zaidi.

Wapongeze watoto kwa kufanya vizuri shuleni au mwenza wako kwa kupendeza na kuwa mke au mume mwema na msaidizi mzuri kwako.

  1. Kuwa Halisia

Unesha uhalisia katika maneno yako na mwonekano wako. Usifanye mambo yaliyo nje ya uwezo wako na yasiyoonesha hali au uwezo wako halisi. Usilazimishe kuishi kitajiri au kisomi wakati sio kweli. Ishi ndani ya uwezo wako na onesha sura halisia kwa watu.

  1. Tabasamu

Tabasamu halimtupi mtu,onesha furaha kwa watu. Tabasamu unapoongea nao na bila shaka watatabasamu pia. Kuna maajabu makubwa katika kitendo hiki. Jaribu leo na uone, kwa kila utakayempa tabasamu ni lazima atafanya hivyo hivyo kwako-ni uhakika.

Tabia za Kupendwa na Watu Zinafundishika

Kupendwa na watu ni jambo muhimu sana katika maisha ya mtu yeyote. Ni muhimu katika utendaji wa majukumu yako ya kila siku iwe kazini,nyumbani kama mwanafamilia na katika mambo mengine ya kijamii na zinafundishika

Ukipendwa na watu ni rahisi kutoa ushawishi juu ya mambo utakayoyatoa kwao. Katika kutafuta masoko,uongozi wa watu au siasa kupendwa na watu ni jambo la muhimu sana.

Fuata mbinu hizi kujenga tabia zitakazokufanya kupendwa na watu siku zote.

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment