Mafanikio

Mbinu 3 Muhimu za Kufanikiwa Kazini

Kufanikiwa Kazini

Umetafuta kazi kwa muda mrefu pengine na sasa umefanikiwa kupata , sasa nini kinafuata?

Bila shaka unahitaji kufanikiwa kazini. Wengine wanapanda ngazi haraka na kufanikiwa ,lakini wengine inawachukua miaka mingi katika safari ya mafanikio. Siri ni nini?

Au umekuwa katika kazi kwa muda mrefu lakini mafanikio yako si makubwa,je unafahamu ni kwa nini?

Makala hii inaelezea namna ambavyo unaweza ukafanikiwa kwa haraka.

Pia Soma: Njia Rahisi ya Kuacha Kazi na Kuanzisha Biashara Binafsi

Kufanikiwa kazini kunatokana na kufanya jambo moja na jambo moja tu kubwa; kuleta athari chanya!
Kuleta athari chanya maana yake ni kuwa utendaji wako ulete mafanikio kwa shirika au kampuni yako. Pia utendaji wako wa kazi ulete faida kwa wafanyakazi wenzako na watu ambao wako karibu na wewe.

Vitu Vitatu Muhimu Katika Kuleta Athari Chanya Kazini
Kuna mambo matatu muhimu ambayo unaweza kufanya ili kupata mafanikio katika kazi na kuleta matokeo mazuri:

  1. Kuthibitisha uwezo wako–Daima tekeleza unachokisema
  2. Kujiamini
  3. Kujionyesha–Fanya watu wakuone na watambue kazi zako

Kwa kufanya mambo haya matatu kikamilifu sio tu utaleta matokeo chanya bali pia utawashawishi watu kuwa wewe ni mtu ambaye watapenda kufanya nao kazi.

1. Kuthibitisha Uwezo Wako

Kufanikiwa-kazini-uwezo

Kuthibitisha uwezo wako ina maana kwamba daima hufanya kile ulichosema utafanya na kwa wakati muafaka. Pia zingatia kanuni na maadili ya taaluma husika.

Hakuna kitu kibaya kama kufanya kazi na mtu ambaye hafanyi kile alichoahidi. Ukishapoteza imani na mtu ni vigumu sana kufanya naye kazi siku za mbele. Zuia kuwa mtu wa aina hii.

Kuthibitisha uwezo wako kwanza ni lazima ujue nini kinahitajika kufanyika kwa ukamilifu.

Njia hizi zitakusaidia kufahamu mahitaji ya kazi yako:

  • Fahamu Tatizo/Fursa

Kabla ya kuanza kazi yoyote , kwanza ni muhimu kujua matatizo au changamoto na fursa zilizomo.

Hii ina maana kuwa ni muhimu kujua matatizo ambayo yanaweza kutokea au fursa pamoja na vyanzo vyake. Mfano kama umepewa mradi ambao umekuwa haufanikiwi, basi kitu cha kwanza iwe ni kufanya utafiti wa kina ili kujua nini kilipelekea kutofanikiwa kwa siku za nyuma. Ukipata sababu,basi itakusaidia sana kuweza kuleta suluhisho.

  • Panga Matokeo ya Kazi Yako

Ukishafahamu chanzo cha matatizo katika kazi yako ni muhimu sana kupanga nini unataka kitokee na katika muda na tarehe utakayopanga.

  • Orodhesha Machaguo Yako

Kwa kuwa sasa unafahamu tatizo au fursa na umeshapanga matokeo unayoyataka sasa unahitaji kufahamu chaguzi zote ambazo unaweza kuzifanya ili kuleta matokeo uliyoyapanga.

Kisha utatakiwa kuchagua moja ambalo ni bora zaidi. Kama chagua la kwanza litashindwa basi utachukua chaguo linalofuata kwa ubora.

  •  Chukua Hatua

Kwa kuwa sasa umeshapanga machaguo yako kinachofuata ni kuchukua hatua na kufanya kama ulivyopanga.

Na uweke mpango wa kufuatilia maendeleo kila mara kuhakikisha kuwa unachokifanya kinaendana na mipango yako na unapata matokeo unayoyategemea.

Utaratibu huu husaidia kwenda polepole au kwa haraka. Mara nyingi tunapopewa kazi ya kufanya huwa tunaingia kichwa kichwa bila kufanya upembuzi wa kutosha na kupanga jinsi ya kuikabili. Utaratibu huu utakusaidia kuleta matokeo mazuri kwa haraka sana na kukufanya uonekane.

 Ni jambo zuri kumuonyesha bosi wako mipango yako kabla ya kufanyia kazi. Hii inamfanya aone kuwa yeye ni sehemu ya kazi hiyo hivyo kutoa masaada wa kutosha katika kufanikisha.

2. Onyesha Kujiamini

Kufanikiwa-kazini-kujiamini

Ni rahisi kuonyesha kujiamini kwako kwa baadhi ya watu na ni vigumu kwa watu wengine. Changamoto uliyonayo ni kiasi gani cha kujiamini kunatakiwa.

Kuwa mwangalifu juu ya kujiamini kupita kiasi, kwani watu watakuona kuwa na maringo na kuonyesha kiwango kidogo cha kujiamini kunaweza kuwafanya watu kukuona kuwa mwenye uwezo mdogo na hivyo kutokutilia maanani.

Kujiamini kwako kunatakiwa kuendane na uwezo wako wa kufanya unachokisema au kupanga. Ukiahidi kufanya kwa kiwango cha juu sana na usifanikishe hukushusha sana na kupunguza uaminifu. Hivyo kiwango cha kujiamini kuendane na uwezo wako.

Kwa kufuata mchakato huu kwa kila kazi unayopewa au kupanga kufanya unakuwa na uhakika kuwa utaifanya kwa mafanikio.Kwa kuwa na mpango wa aina hii unakuwezesha kuweza kuwashirikisha watu wengine kwa urahisi akiwemo bosi wako na hivyo kuongeza imani juu yako.

3. Kujionyesha (Kuonyesha Ufanisi wa Kazi Zako)

Kufanikiwa-kazini-jinadi

Kuonekana katika utendaji wa kazi zako hutegemea sana na mafanikio ya kazi zako  na jinsi unavyojiamini.

Siri ya kuonekana kwako katika kazi kunategemea jinsi ambavyo wewe mwenyewe unavyojinadi na kuwaonyesha watu unachokifanya kwa ufanisi.

Kumbuka hakuna anayempenda mtu anayejiamini kupita kiasi, ambaye anatumia muda mwingi kujinadi na kujigamba badala ya kuonyesha matokeo,hali kadhalika hakuna mtu atakayemuona mtu ambaye hajiamini na asiyeweza kuonyesha ufanisi wake wa kazi.

Jinsi gani unaweza kujinadi mwenyewe?
Kujinadi kazini ni sayansi na sanaa. Kitu cha muhimu katika kufanya hivyo ni kwa kuzingatia nini umefanya na sio wasifu wako binafsi.

Kwa kuonyesha vitu ulivyofanya kwa mafanikio vitawavutia watu zaidi kuliko kwa kuwaeleza wasifu wako binafsi.

Mbinu hizi zitakusaidia kujinadi kazini:

  • Ainisha vitu ambavyo umevifanya na vimeleta mafanikio kazini kwako.
  • Ainisha ni watu gani wanahitaji kufahamu-Hawa ni watu muhimu kazini kwako ambao wanahitaji kufahamu na kwa kujua kwao kunaweza kuleta athari.
  • Panga Utakavyowajulisha-Ni jinsi gani watu aliopanga wafahamu watajulishwa kuhusu kazi zako.

Kwa kufanya mkutano na kutoa taarifa,au kwa kuwaandikia barua-pepe au kwa kumweleza mtu moja mmoja

Mwisho…

Kwa kumalizia,ni kwamba sifa yako na mafanikio makubwa katika kazi yatatokana na kufanya kazi zako kwa ufanisi.

Meneja mzuri anahitaji watu bora katika timu yake, na watu bora ni wale ambao wanafanya nakutimiza kile walichosema na wale ambao wanajituma kwa uwezo wao wote ili kuleta mafanikio kazini na kufanya mafanikio yao yaonekane kwa wengine.

Hivyo kama unataka kufanikiwa kazini na kuleta athari chanya, basi hakikisha unaonyesha uwezo ulio nao,unaonyesha kujiamini kulingana na uwezo wako na unanadi uwezo na ufanisi wa kazi zako

 Je wewe unatumia mbinu gani  ili kufanikiwa kazini kwako?

Tueleze kwa kuandika katika kisanduku cha maoni chini ya makala hii na uitume.

 

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment

2 Comments