Mafanikio

Kwanini Mipango na Maazimio ya Mwaka Mpya Hayafanikiwi?

Mipango na Maazimio ya Mwaka MpyaNi kawaida kwa walio wengi kuweka maazimio na mipango kila mwaka unapoanza,au hata katikati ya mwaka. Jiangalie mwenyewe kama mfano,malengo yako ya mwaka uliopita yamekamilika? Je kwa kiasi gani?,utagundua si kwa kiwango cha kuridhisha sana.

Watu wanakuwa na shauku kuubwa ya kupanga na kutekeleza mipango yao lakini mipango mingi haitekelezwi. Sababuni nini? Utajiuliza. Katika makala hii tutaangalia sababu saba (7) kubwa zinazofanya malengo ya mwaka yasikamilike.

Pia Soma: Namna ya Kuanza Mwaka Mpya Kwa Fikra Mpya za Mafanikio

Sababu Kuu 7 Kwanini Mipango na Maazimio ya Mwaka Mpya Hayafanikiwi:

1. Malengo kuwa Makubwa na Mapana Sana

Malengo yanakuwa makubwa na yasiyo na uhalisia. Ili malengo yatekelezeke yanatakiwa kuwa na sifa kuu  tano (5) zifuatazo:

  • Yawe wazi,maalumu na yasiyo na mkanganyiko: Lengo linatakiwa kuwa rahisi na lenye kueleweka
  • Yapimike: Yaani katika kipindi fulani uweze kupima maendeleo wapi imefikia. Namba ni muhimu. Mfano kununua mashamba mawili katika miezi 6 ya mwaka husika.
  • Yenye kufikika: Malengo yako ni lazima yawe halisia na yenye kuwezekana. Huwezi kuweka lengo mfano “Kujenga nyumba 5 katika mwaka mmoja wakati kipato chako cha mwezi hakioani nanma malengo hayo”
  • Yenye uhalisia: Malengo yawe halisia na siyo ya kufikirika tu. Nataka kujenga ghorofa mwaka huu, wkati hata hela ya kula nyumbani inasumbua.
  • Yenye muda maalumu: Ni lazima uweke muda wa kutimiza lengo au jambo ulilopanga.

2. Kutaka Kufanya Mambo Mengi kwa Mara Moja:

Kutaka malengo ya maisha yako yote au ya miaka 10 yafanyike katika mwaka mmoja,ni jambo lisilowezekana. Na wengi tunashindwa hapa. Ni lazima kuangalia uwezo wakutekeleza mipango hiyo katika kipindi husika.
Malengo mengi tunayoweka ni matamanio yetu katika maisha. Ni vitu ambavyo tungependa vitokee au tuvikamilishe katika maisha yetu.

3. Kutokuwa na Mpango wa Utekelezaji:

Kila lengo ni lazima litengenezewe mpango wa kulitekeleza. Hapa utavunjavunja kila lengo katika kazi ndogondogo na kuzipangia muda kwa kila kazi pamoja na muhusika (nani atakayefanya) na mahitaji yake ya kuikamilisha. Lengo linaweza kuwa kubwa sana na lisilotekelezeka mpaka utakapoweza kulikatakata katika vipande vidogo vidogo.

4. Kukosa Mkazo na Msukumo:

Hili linaweza kutokea ukiwa na malengo mengi kupita kiasi. Ambapo utashindwa kutulia katika lengo moja na kupata matokeo. Badala yake utakuwa unafanya nusu ya hili na nusu kwingine pia na hatimaye hutatimiza hata moja.

Unapokuwa hufanikishi kazi yoyote unakosa msukumo wa kufanya mengine pia na kufa moyo.

5. Kutoandika na Kutorudia Kuyasoma Malengo Yako:

Iwe unaandika au unatunza kichwani ni muhimu sana kuyarudia malengo yako kila mara. Wataalamu wanashauri uyasome kila siku asubuhi ,mchana na jioni.

Tembea nayo kila unakoenda na kamwe usiachane nayo. Unaporudia kusoma malengo yako yanawekwa kwenye mawazo au akili ya kina  ambayo inauwezo mkubwa wa kukusukuma kukamilisha malengo hayo. Soma makala kuhusu Nguvu ya Mawazo ya Kina hapa

6. Kutoshirikisha Wengine:

Njia nyingine ni kushirikisha wengine, mfano mwenza wako au marafiki au wazazi n.k. Hawa watakukumbusha pale unapojisahau. Mipango ya mtu mmoja haina nguvu na ni rahisi kuiacha kabla ya kufikia mwisho. Pale unapowashirikisha wengine mwili na akili yako inakuwa imejipa jukumu ya kuhakikisha inatimiza,linakuwa kama deni kwako ambalo ni lazima ulilipe.

7. Kutopima Maendeleo Mara Kwa Mara

Ni muhimu kuyapitia malengo yako na kuyapima mara kwa mara. Angalia kila baada ya mwezo mmmoja mfano,je umefikia wapi? Umweka hatua za kuridhisha? Na kama siyo,changamoto ni nini ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi na kuweza kwenda mbele.

Kupima maendeleo katikati ya mwaka ni muhimu sana kuweza kufanikisha malengo yako ya mwaka. Kama huwezi kufanya kila mwezi,basi angalau kila baada ya miezi mitatu(3),hii itasaidia kujitahmini na kukupa nguvu za kusonga mbele kwa haraka.

Hitimisho:

Je kuna sababu nyingine zinazofanya malengo na maazimio ya mwaka mpya yasifikiwe? Tafadhali ongezea katika kisanduku cha maoni hapa chini.

Bila shaka makala hii itakupa mwanga na mwongozo pale unapoandika maelengo yako ya mwaka mpya ili hatimaye ufanikiwe kwa kuyatimiliza.

Nakutakia heri na mafanikio kwenye mipango yako mipya ya mwaka.

Kama makala hii imekufaa na umeipenda,basi sambaza upendo kwa kubofya vitufe hapo chini kwenda mitandao ya kijamii.

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment