Michezo Utamaduni

Muziki wa Bongo Flava:Unaweza Kuwa Utambulisho wa Utamaduni wa Tanzania

bongo-flava

Historia ya Bongo Flava

Muziki wa Bongo Flava unachukuliwa kuwa na asili ya Tanzania,japo ulikirudi nyuma utagundua muziki huu ulikuwa wa kuiga muziki wa nje hasa kutoka Marekani wenye vionjo vya Kufokafoka yaani “Rap”.

Tunakumbuka bendi ya Mawingu miaka ya 90 na wengine kama Mr II-Sugu ,Kwanza Unit,HardBlasters na Brofesa J,Wagumu Weusi,Sostenes Amabakisye “Sos B” na wengine wengi wanachukuliwa kuwa waanzilishi wa muziki wa Bongo Flava.

muziki-wa-bongo-flava_sugu-3

II Proud au Mr II – “Sugu” ni mojawapo ya waanzilishi wa Bongo Falava na Hip Hop ya Bongo

muziki-wa-bongo-flava_hardblasters

Joseph Haule “Profesa J” na kundi lake la Hard Blasters walichangia sana katika kukuza Bongo Flava na Hip hop ya Bongo

Sehemu kubwa ya nyimbo za Bongo Flava wakati huo zilikuwa za kukopi zikiwa zimebadilishwa lugha tu na pengine kuweka misemo michache ya kiswahili.

Muziki huu haukupokelewa kwa shangwe sana na watanzania hasa wazee,ulionekana kuwa ni wa kihuni,labda kutokana na mashairi ya kukopi toka kwa wamarekani na kukosa maudhui kwa jamii ya Kitanzania.

Hauikutegemewa kuwa Bongo Flava ingeishi kwa muda mrefu,lakini kwa sasa imekua na kila mtu anaweza kuona. Imepitia katika hatua kadhaa za mabadiliko na sasa ina wapenzi wengi tena wa rika zote wakiwemo hata wazee.

Fursa ya Kukuza na Kutangaza Utamaduni wa Tanzania

Bongo Flava inapendwa na watu hata nje ya mipaka ya Tanzania. Kenya,Burundi,Rwanda na hata Marekani na Uingereza. Hii ni fursa ya kujitangaza na kuutangaza utamaduni wa Tanzania na Afrika.

Serikali kupitia wizara husika iweke mikakati katika kukuza na kuendeleza muziki wa Bongo Flava kwa kuweza mazingira mazuri kwa vijana kujiajiri na hupata maendeleo binafsi na kwa taifa kwa ujumla.

Serikali kupitia vyombo vyake kama Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA) kuweza kusimamia haki za wanamuziki hawa.

Pia kuwekwe masharti katika utengenezaji wa nyimbo hizi kama vile kutotumia lugha za matusi na kutumia kiswahili ambacho ni fasaha. Kwani hii ni fursa ya kukuza utamaduni wetu kupitia lugha yetu ya kiswahili.

muziki-wa-bongo-flava_diamond-1

Diamond ni mojawapo ya wanamuziki wa Bongo Flava nchini Tanzania anayewika sana na anajulikana hadi nje ya mipaka ya Tanzania

muziki-wa-bongo-flava_ali-kiba-1

Ali Kiba ana kipaji kikubwa cha kuimba na amechangia sana kuendeleza Bongo Flava. Ameshirikishwa na wasanii wakubwa wa nje

Vitu Ambavyo Vitafanya Muziki wa Bongo Flava Kuwa Kitambulisho cha Taifa:

Muziki huu uweke vitu kadhaa ambavyo vitabeba utambulisho wa kitaifa, na serikali pamoja na kusimamia haki zao lakini wahakikishe kuna wanamuziki wote wanafuata taratibu za msingi katika kuandaa nyimbo zao.

Vifuatavyo ni baadhi ya vipengele muhimu vya kuzingatiwa

  1. Midundo na Ala za Muziki

Japo ala za Bongo Flava nyingi zinatengenezwa katika kompyuta na sio upigaji wa vyombo moja kwa moja lakini iwekwe midundo ya kitanzania kama marimba ya kimakonde na filimbi. Midundo ya ngoma toka makabila mbalimbali ya tanzania yasikike katika kila muziki wa Bongo Flava.

  1. Vibwagizo vya Kiasili

Kuwekwe vibwagizo vya sauti za kiasili,hata ikiwa sehemu ndogo tu ya muziki.

Kumbuka mwanamuziki maarufu wa muziki wa pop duniani Marehemu Maiko Jackson aliimba kiswahili japo sentensi moja tu katika wimbo wake wa “Liberian Girl” aliimba maneno “Napenda pia,nakutaka pia” japo wimbo hupo ulikuwa wakiingereza. Vibwagizo vya aina hii vinaweza vikachanganywa katika miziki yetu hasa Bongo Flava.

  1. Mavazi ya Kiasili ya Kitanzania katika Video

Nyimbo nyingi sasa hivi zinaendana na utengenezaji wa video,hivyo mandhari ya kutengeneza video hizo yaakisi utamaduni wa Kitanzania. Mavazi ni kitu muhimu hapa kwani ni mojawapo ya nguzo kuu ya kutambulisha utamaduni.

Ni vyema kufahamu hapa kuwa wanamuziki wetu wanapoenda kuimba nje kama Ulaya na Marekani,watu wa kule wanapenda kuona Afrika au tanzania inafanana vipi? Hivyo Uvaaji wako na lugha ni vitu muhimu kuzingatiwa katika maonyesho hayo. Kama unawapigia miziki kama ambavyo wanamuziki wao huko wanapiga utapataje kupendwa?

  1. Ujumbe na Kufuata Kanuni za Ushairi

Kazi za wasanii wetu zifuate kanuni za muziki,uumbaji wa maneno na mashairi yake. Vina na mizani ni mojawapo katika vitu vya kuzingatiwa ili kutengeneza kazi yenye ufanisi wa kisanaa.

Ujumbe katika nyimbo pia izingatiwe ili kuweza kuvutia watu wa rika zote na wenye mitazamo tofauti juu ya maisha.

 

Faida Kijamii na Uchumi:

Kama mambo haya yaliyoainishwa hapo juu yatafanyika na muziki huu kupewa umuhimu unaotakikana,ni wazi utasaidia kutangaza utamaduni wa Tanzania na hata kukuza pato la taifa kwa kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi.

Pia muziki wa Bongo Flava utaendelea kutoa ajira kwa vijana na hata watu wazima na kupunguza janga na wananchi wake kukosa ajira na hivyo kuleta ustawi wa jamii.

Je wewe una mtazamo gani juu ya muziki wa Bongo Flava? Unafikiri vitu gani zaidi vifanywe ili kuuboresha na kuwa utambulisho wa Taifa?

Tuandikie Maoni yako katika kisanduku cha maoni hapa chini ya makala hii.

 

 

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment