Fedha na Uchumi

Namna ya Kuendesha na Kupunguza Matumizi ya Mafuta ya Gari

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-0

Matumizi ya gari ni mojawapo ya matumizi makubwa kwa familia nyingi hasa zinazoishi mjini.

Inasemekana kwa wale wanaomiliki magari kuwa inawezekana nyumbani kukakosekana baadhi ya mahitaji mengine muhimu lakini gari ni lazima liwekwe mafuta na litembee. Je kuna ukweli wowote? Jaribu kufanya utafiti utaona. Watu wanalalamika uchumi mbaya lakini magari yanatembea.

Hii inamaanisha kuwa kwa maisha ya kisasa tunayoishi gari limekuwa mojawapo ya nyenzo muhimu na ya lazima. Lakini pia ni mojawapo ya kitu ambacho kinakula fedha nyingi toka mifukoni mwetu.

Kila mtu anatakiwa kutafuta jinsi ya kupunguza matumizi yamayotokana na gari. Mafuta ni sehemu mojawapo ya matumizi makubwa katika kumiliki nakuendesha gari.

Katika mada hii tunaangalia mbinu za kupunguza matumizi ya mafuta ya gari hivyo kuboresha uchumi wa wamiliki. Kuna usemi unaosema “Shilingi uziyookoa ni sawa na shilingi uliyoingiza”.

Mbinu za Uendeshaji Zinazosaidia Kupunguza Matumizi ya Mafuta ya Gari

Madereva wengi wanaendesha magari kwa namna ambayo inasababisha injini kula mafuta mengi sana. Kama utaendesha gari kwa kufuata mbinu hizi tu unaweza kupunguza matumizi yako ya mfuta kwa asilimia 10-20.

 1. Zingatia Mwendo Kasi Sahihi

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-spidi

Kila gari linatumia mafuta katika namna tofauti, lakini katika spidi juu ya 90 Km/Saa mpaka 100 Km/Saa gari lolote huwa linatumia mafuta kidogo kuliko likiwa katika spidi nyingine. Kwa mjini huwezi kufikia spidi hii lakini jitahidi kuendesha juu ya 30 Km/Saa.

Pia fahamu kuwa spidi ikizidi 50Km/Saa mafuta yatatumika zaidi kwa kuwa gari linahitaji nguvu zaidi kushindana ukinzani wa hewa.

Zingatia: Zuia mwendo kasi kati ya 60-90 Km/Saa kwakuwa hutumia mafuta mengi

 1. Usiongeze Mwendo Kwa Haraka

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-oneza_spidi

Kukanyaga mafuta kwa haraka ilikuongeza spidi kunachangia ulaji mkubwa wa mafuta. Unashauriwa kukanyaga mafuta taratibu unapoongeza mwendo kasi.

Unaweza ukasikiliza gari lako wakati unaendesha,ukisikia sauti kubwa unapoongeza mwendo ujue unachoma mafuta mengi na hivyo unaongeza gharama.

 1. Usipunguze Mwendo Kwa Haraka- Acha Ukanyagaji Breki za Kushitukiza

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-breki

Kama ilivyo katika kuongeza mwendo,unatakiwa kupunguza mwendo taratibu. Hakikisha kuna umbali wa kutosha kati yako na gari la mbele yako vinginevyo utajikuta ni lazima ukanyage breki kwa haraka na kwa kushitukiza ambako kunasababisha injini kula mafuta zaidi.

 1. Kutobeba Mizigo Mizito Kwenye Gari

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-mizigo

Uzito unapoongezeka katika gari hufanya injini kutumia nguvu nyingi kusukuma gari na hivyo kuhitaji mafuta mengi zaidi. Punguza mizigo isiyo ya lazima katika gari ukiwa unaendesha.

 

 1. Kutoacha Gari Likiwa Linawaka Bila Kutembea

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-paki-1

Utafiti unaonesha kuwa kwa wastani gari linatumia lita zipatazo 2 kwa saa kama likiwa linawaka bila kutembea. Sababu ni kuwa katika hali hii injini huwa inatembea na inahitaji mafuta kuzunguka.

Kama gari halitembei unashauriwa kuzima injini ili kupunguza matumizi ya mafuta.

Zingatia: Usiache gari likiwa linawaka zaidi ya dakika 1 bila kutembea

 1. Zima Kiyoyozi (AC) Katika Mwendo Mdogo

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-ac

Katika mwendo kasi wa chini ya 90 km/saa zima kiyoyozi na fungua madirisha. Kiyoyozi kinazungushwa na injini hivyo kutumia mafuta zaidi. Kukiwa unaenda spidi zaidi ya 90km/saa unatatumia mafuta kidogo ukifunga madirisha na kuwasha kiyoyozi.

 

Katika mwendo kasi mkubwa ukinzani wa upepo unaongezeka madirisha yakiwa wazi na kufanya injini iwe na mzigo mkubwa kusukuma gari kwenda mbele.

 

 1. Tumia OD (Over Drive) Kwa Usahihi

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-OD

Swichi ya OD imo katika magari mengi. Swichi hii ikiwashwa inafanya gari kwenda katika gia ya juu na hivyo kupunguza mzunguko wa injini wakati spidi ikibaki juu. Hivyo kupunguza ulaji wa mafuta. Utahitaji kuzima pale ambapo utatakiwa kuongeza nguvu ya gari na kushuka gia ya chini.

 

Ni rahisi kulazimisha gia ya juu au chini kama gari lako ni Manual,vinginevyo ni ngumu kuchagua gia ipi utumie katika mwendo mdogo kama gari yako ni Automatic.

 

OD pia inasaidia kupunguza ulaji wa mafuta na kulika kwa breki unapohitaji kupunguza mwendo kasi kwa kuwa injini inakuwa ikizunguka kwa kasi ndogo.

 

 1. Endesha Gari Likiwa na Matairi Yenye Upepo wa Kutosha.

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari_upepo-wa-tairi

Matairi yenye upepo mdogo yanasababisha kuongezeka kwa eneo linalokanyaga barabara na hivyo nguvu nyingi inahitajika kusukuma gari.

Hakikisha matairi ya gari lako yana upepo katika viwango sahihi.

 

 1. Zuia Kuendesha Gari Katika Foleni Ndefu

kupunguza-matumizi-ya-mafuta-ya-gari-foleni

Gari linatumia mafuta zaidi katika foleni zisizoenda. Chagua njia isiyo na foleni hata kama ni ndefu zaidi. Pia unaweza kuamua kusafiri wakati foleni zimepungua au hazijaanza. Asubuhi sana,mchana na usiku.

 

Mambo Mengine ya Kuangalia

Katika mazingira mengine utahitaji kuruka baadhi ya mambo niliyoyaorodhesha hapa ili kupata faida ya kitu kingine. Mfano Katika mji ambao una joto kali kama Dar es Salaam ,AC ni kitu cha muhimu. Binafsi pia huwa nawasha AC muda wote na naendesha kwa starehe zangu.

Jambo jingine ni spidi ,katika mazingira mengine spidi kubwa au ndogo ni muhimu kulingana na uharaka wako wa safari hivyo huenda usifuate kuokoa mafuta na ukakosa mambo ambayo yanaweza kuwa muhimu zaidi.

Madereva Wengi Wanakiuka Masharti ya Uendeshaji Mzuri

Kwa kumalizia niseme tu kuwa ukiangalia mambo haya tisa niliyoyandika juu ya kupunguza matumizi ya mafuta ya gari utagundua kuwa madereva wengi wanafanya makosa makubwa katika uendeshaji ambayo yanaongeza matumizi ya mafuta na gharama binafsi na kwa familia au kampuni.

Toa mchango wako kuhusu uzoefu wako katika hili. Pia kama una mawazo tofauti katika baadhi ya mbinu tajwa basi tuandikie katika kisanduku cha maoni hapo chini ili tuelimike zaidi.

Asante kwa kusoma na nakuoma ujisajili katika kisanduku kulia kwa ukurasa huu ili upate makala kama hizi kila tunapoandika.

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment

3 Comments

 • umetoa elimu nzuri sana, isipokuwa natofautiana na wewe katika suala la Spidi.Ukweli wa kisayansi (Phyiscs) unasema kuwa “nguvu zaidi,nishati zaidi/spidi zaidi,nishati zaidi”.huwezi kuendesha gari katika spidi ya 90/100KM/pH halafu uwe chini ya 2.5 R/pM (rpm).

  mara zote mshale wa rpm unaenda sawa na mshale wa spidi.msingi ni kuwa “rpm kubwa,spidi kubwa na mafuta mengi”.kama uko makini katika kubadilika kwa gia za gari (kama gari yako siyo ya CVT gear box) utagundua kuwa unapofika spidi ya 90KM/pH gari huwa inashtuka,hiyo maana yake ni kuwa valve zote zimefunguka kwa sababu hapo gari huwa inatembelea Gia namba 5

  Katika elimu yako nzuri sana uliyotoa,hongera, wewe umeenda kinyume.

  ukweli ni kuwa madereva wa magari madogo ni lazima wayaendeshe katika spidi ya 50KM/pH mpaka 80KM/pH kwa sababu hapo gari itatembea katika Gia namba 3 au 4 na dereva makini ataitunza rpm ya 1.5 mpaka 2.0.maana yake ni kwamba gari itatembea katika rpm inayotumia nishati kidogo na zaidi ya yote itakuwa katika gia namba 4 ambayo kisayansi haifungui valve zote katika injini.

  Madereva waepuke sana spidi chini ya 50KM/pH kwa sababu mara nyingi spidi hizo hutumia si zaidi ya gia namba 2 katika mpishano,sayansi inasema kuwa gia inapokuwa ndogo injini inakuwa na nguvu mno lakini inakosa spidi na ndo mana milima mikali huwa inapandwa na gia namba 1 au L katika gia ya automatiki,aidha gia ya kurudia nyuma “R” ndiyo gia yenye nguvu kuliko zote na ndiyo ambayo haina spidi kuliko zote kwa sababu ndo gia ndogo kuliko zote.

  fomula inasema “gia ndogo,nguvu kubwa,spidi ndogo” na “gia kubwa,nguvu ndogo,spidi kubwa”.hivyo ukitunza gia namba 3 mpaka 4 (50KM/pH-80KM/pH) katika kuendesha utatunza sana mafuta yako kwa sababu rpm itakuwa chini na valve havitafunguka zote. gia namba 5 (90KM/pH na kuendelea) utakula mafuta mengi kwa sababu rpm itakuwa juu na valve zote zitafunguka ili zikachome nishati kwa wingi ili gari ikimbie sana.

  THANX

 • Benini,
  Asante kwa maoni yako. Nikushukuru kwani umedadavua vizuri. Nitaomba nikupe mada hapa za kuandika kuhusu sayansi na teknolojia ya magari.

  Nakubali kuwa gari litatumia mafuta mengi katika spidi ya 90km/saa kuliko 50-80km/saa japo pia itategemea na aina ya gari pia mzigo ambao gari limebeba.
  Lakini ukiwa katika safari ndefu pia ni vigumu kuendesha katika spidi chini ya 80km/saa na katika mazingira hayo basi nafikiri spidi ya 90-100km/saa itafaa zaidi.

  Pili kutokana na sayansi ya fizikia, gari likiwa katika spidi kubwa,momentum inakuwa kubwa (momentum ni msukumo wa kwenda mbele kulingana na uzito wa chombo) hivyo inasaidia kusukuma gari bila nguvu kubwa sana ndio maana pia katika spidi ya 80-100 km/saa unaweza kutumia mafuta kidogo. Zaidi ya hapo ukinzani wa upepo unaongezeka sana na kusababisha kutumia mafuta zaidi na itakuongezea gharama.

  Binafsi nikienda safari ndefu najaribu kubaki kati ya 90-100 km/saa.

  Hata hivyo nakubaliana na maoni yako,mimi pia nimejifunza toka kwako.
  Asante

 • Natanguliza shukran kwako, na kwenu nyote ktk kuchambua na kudadavua somo hili. Naomba kujuwa iwapo nitaendesha ktk 3.5 rpm kwa mwendo wa km 20 nitakuwa nimeokoa mafuta?