Biashara na Ujasiriamali

Namna ya Kutengeneza na Kuuza Mpango Biashara

Kuuza Mpango Biashara-3

Ili kuanzisha na kuendesha biashara kwa mafanikio ni lazima uwe na Mpango Biashara utakayokupa dira ya biashara yako. Kama una mawazo mazuri ya kuanzisha biashara itakayofanikiwa basi unaweza kuandika na kuuza Mpango Biashara kwa watu ambao wana fedha za kuwekeza katika biashara hiyo

Mpango Bisahara ni andiko ambalo huelezea jinsi biashara yako itakavyoendeshwa. Inaelezea kwa ujumla bidhaa au huduma unazotarajia kuuza,ubora wa bidhaa hizo au huduma utakazotoa,mtaji unaohitajika na wapi utapata,matarajio ya mauzo katika kipindi utakachotaja,inaweza kuwa mwaka mmoja ,mitatu au mitano.

Pia unaelezea nani atafanya kazi ya kuuza au kutafuta masoko,ushindani na jinsi ya kukabiliana nao,jinsi utakavyopata masoko nk.

Kwa bahati mbaya si watu wengi wanajua kuandika mpango huu,na hata wale wanaojua hawafanyi,nachelea kusema kuwa hii ni mojawapo ya sababu ya kushindwa kwa biashara nyingi mpya na hata zile zinazoendelea.

Mpango Biashara ni muhimu unahitajika sana kwa biashara mpya na hata zile zinazoendelea.

Si Kila Mtu Anaweza Kubuni Biashara

Kuna pengo kubwa kati ya watu wenye fedha za mitaji na wale ambao wana mipango mizuri ya biashara yenye mafanikio lakini wanakosa fedha za mitaji.

Benki kwa mfano, wana fedha lakini zinahitaji watu au makampuni yenye mipango thabiti ili waweze kuwakopesha.

Hali kadhalika matajiri wakubwa wanaohitaji kuwekeza fedha zao ili zizae zaidi.

Tunaona makundi wawili hapa:

 1. Kundi la watu wenye fedha lakini hawana mipango mizuri au wanaohitaji mipango mizuri ya biashara
 2. Kundi la wenye mipango mizuri ya biashara au wale ambao wanaweza kubuni mpango mzuri wa biashara na kusimamia lakini hawana fedha za mitaji

Sasa dhumuni la mada ya leo ni kuangalia fursa ya kuunganisha makundi haya kwa faida ya pande zote mbili,wenye fedha wawekezaji na wataalamu wa uongozi wa biashara au wale wenye mpango wa biashara lakini wasio na fedha. Hapa kuna fursa kwa wale wasio na fedha za mitaji lakini wana mawazo mazuri ya biashara kuandika na kuuza mpango biashara kwa wenye fedha.

Ubunifu ni Kipaji cha Kuona Mbali na Kuota Ndoto

Kuuza Mpango Biashara-ubunifu

Kuwa mbunifu wa vitu vizuri ni kipaji ndio maana si kila mtu anaweza. Ubunifu unahitaji mtu ambaye anaweza kuwa na maono ya mbali ya vitu ambavyo hata havipo bado kwa kujenga taswira na kuhamishia katika kitu halisia kinachoonekana kwa macho na kushikika.

Mtaalamu wa falsa za fikra na muandishi maarufu Napoleon Hill anasema hivi “Kama unaweza kufikiri juu ya kitu fulani,basi unaweza ukakipata au kukifanya kuwa kweli” .

Mawazo yako yanaweza kuwa kweli. Uvumbuzi wowote mkubwa duniani ulianza kwa mawazo na hatimaye kutimilizika katika vitu halisi.

Inasemwa kuwa kama unataka kujenga nyumba ni lazima iwe imesha kamilika mawazoni mwako kwanza kabla hujaweka tofali la kwanza.

Hivyo kuna wale wenye uwezo wa kutumia kalama hii kufikiri na kubuni biashara ya mamilioni ya fedha na zenye kuleta faida kwa wamiliki. Lakini kwa upande mwingine kuna wale wasio na uwezo huu.

Tukiwakutanisha watu hawa na wakaaminiana na wakafanya kazi kwa ushirikiano na kuaminiana basi maendeleo ya pamoja ni jambo la kutegemewa.

Jinsi ya Kubuni Biashara,Kuandika na Kuuza Mpango Biashara kwa Wawekezaji

Ili kutengeneza Mpango Biashara wenye kuuzika kwa watu ni lazima uandikwe katika ustadi wa hali ya juu na yenye kuzingatia vitu kadhaa muhimu, hapa tuangalie vitu vinne muhimu:

# 1: Mahitaji ya Watumiaji au Walaji

Kuuza Mpango Biashara-mahitaji

Ubunifu wa biashara unakuja kwa kuangalia mahitaji ya jamii, biashara yoyote ambayo inalenga kutoa huduma au bidhaa ambayo inahitajika katika jamii ni lazima itafanikiwa. Mara nyingi watu wanabuni biashara ambayo inatoa huduma nzuri tu au bidhaa za thamani na ubora lakini bila kuangalia mahitaji na uwezo wa kununua wa watumiaji. Hivyo kitu cha msingi katika ubinifu wa biashara yenye faida ni kuangalia mahitaji na uwezo wa kununua wa jamii watumiaji.

# 2: Andika Mawazo Yako

Kuuza Mpango Biashara-andika

Ni sharti kuandika mawazo yako, kuna faida kubwa sana ya kuandika mawazo yako mojawapo ni kuwa mawazo ya kibunifu huwa yanakuja kwa wakati fulani tu na si wakati wote,lakini pia kuna maajabu makubwa yanatokea katika fikra zako unapokuwa na karatasi na kalamu mbele yako,utashangaa jinsi ambavyo unaweza kuandika vitu vingi kiasi ambacho usingeweza kama usingeandika.

Mwalimu wangu wa falsafa za maisha Brian Tracy anasema hivi “Kama kitu hakijaandikwa basi hakipo”. Yaani mawazo yako hata yakiwa ya ubunifu kiasi gani lakini hayakuandikwa basi ni kazi bure. Ni rahisi kuwashirikisha watu wengi mawazo yaliyoandikwa kuliko fikra katika kichwa chako pekee.

 #3: Yasajili Mawazo yako na Upate Haki Miliki

Kuuza Mpango Biashara-umiliki-1

Hiki ni kitu kipya hasa Afrika. Mawazo ya kibunifu yaliyoandikwa na yaliyofanyiwa uchunguzi kuwa na faida kwa jamii yanaweza kumilikishwa kwamhusika na kuzuia wizi wa mawazo.

Hili linakufanya wewe uliyeandika kwa mara ya kwanza kuwa mmiliki pekee wa mawazo hayo.

Nchini Tanzania kuna Tasisi ya Kuangalia Haki na Hati Miliki ijulikanayo kama COSOTA na BRELA

Tafadhari peleka mawazo yako ya kibunifu huko yasajiliwe na upate hati ya umiliki

# 4: Yanadi Maandiko yako Yenye Umiliki

Kuuza Mpango Biashara-nadi-3

Kinachofuata ni kutafuta taasisi ,mashirika na watu binafsi wenye fedha na unadi maandiko yako ya biashara.

Unaweza ukaomba mkopo binafsi ambao utarejeshwa au uwaweke kama wamiliki wenza (Share Holders)

[Soma: Mbinu za kupata mtaji wa biashara]

Ni rahisi kupata fedha kwa namna hii na ukafanya mwenyewe uongozi wa biashara hiyo au ukaiuza tu bila ya kuaka wewe mwenyewe kuiendesha.

Unaweza kupata fedha nyingi kwa kuandika mawazo pekee na kuwauzia wengine ambao wataziendesha kadiri ya ilivyoandikwa

Hitimisho:

Kwa namna hii basi tunaweza kuona soko jipya la biashara ya kuuza mawazo tu, andika,pata hati miliki,uza.

Lakini pia unaweza kutumia maandiko haya kuomba mitaji ya biashara na kuziendesha mwenyewe kama Mkurugenzi Mtendaji au mmiliki.

Haya basi ndugu,anza leo kuandika kila wazo zuri lipitalo kichwani kwani ni mali yenye thamani kubwa.

Andaa,kitabu cha mawazo bunifu leo na tumia dakika kama 30 kila siku kufikiri na kuandika kitu chenye manufaa.

Tafadhari changia juu ya mada hii ya kuandika na kuuza mpango biashara ili kuboresha zaidi,andika maoni yako hapa chini na ushiriki

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment

2 Comments

 • Nimeburudishwa sana na ukurasa huu maana naona ni kama karibuni nitapata upenyo, maana ninamipango debe inaoza tu na hata nimeshasajili kampuni lkn sina mtaji wa kuiendesha, mnasemaje kuna utaratibu maalumu tuanze kuongea au yote ni hapa tu.

  • Ndugu Justous,Kwanza asante kwa kusoma makala zetu. Wakaribishe wengine pia ili wafaidike.
   Bongo Posts tunaandika habari ili kuelimisha na tunategemea watu kuchukua hatua wenyewe. Mfano kama una mipango katika kabati basi tafuta mtu ambaye atakuwa na nafasi ya kuungana nawe ili kufanya biashara kama ulivyoiandika.

   Lakini pia unaweza kuomba mkopo benki au katika taasisi ndogo ndogo za mikopo ikiwemo vikoba kutumia mipango yako ambayo tayari ipo katyika maandishi.

   Lakini unaweza ukaongea nasi pia kwa simu na barua pepe kupitia ukurasa wa Mawasiliano katika tovuti hii hapo juu kwa mawazo zaidi.

   Asante.