Mafanikio

Namna ya Kutumia Fikra za Kina Kuleta Matokeo Makubwa Katika Maisha

kutumia-fikra-za-kina-1

Kuna utofauti mkubwa kati ya elimu ambayo binadamu anapata katika maisha yake na matumizi ya elimu hiyo katika kuleta suluhisho za mambo mabalimbali katika maisha yetu. Tunatumia robo mpaka nusu ya maisha yetu katika kutafuta elimu lakini kiasi kidogo sana cha elimu tulizojilimbikizia vichwani mwetu inatumika katika maisha ya kila siku.

Sababu kubwa ni kuwa matendo yetu yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia na hisia zetu na sio elimu tulizonazo na kama tukiweza kubadili hali hii na kuanza kutumia elimu zetu katika kila tunachofanya basi matokeo yake yatakuwa makubwa sana.

Kutumia fikra za kina badala ya fikra za ufahamu ni suluhisho la tatizo hili kwani fikra za kina zinachukua 90% za uwezo wa binadamu na 10% tu inachukuliwa na fikra za ufahamu  ambazo ndizo zinazohusika na  elimu.

Aina Mbili za Fikra za Binadamu

Kuna aina kuu mbili za fikra katika mwili wa binadamu ambazo zinaongoza maisha yake, Fikra za Kawaida(Ufahamu) na Fikra za Kina.

kutumia-fikra-za-kina-2

1. Fikra za Kawaida au Fikra Fahamu (Conscious Mind)

Fikra Fahamu ni sehemu ya akili yako inayofanya kazi ya kutunza utambuzi ,mantiki na kuhoji mambo. Ukiulizwa moja jumlisha moja ni ngapi hutumia akili hii kutoa majibu.

Pia huongoza vitendo vyote ambavyo unavifanya wakati ukiwa na fahamu. Kwa mfano, kutembea,kuammua juu ya kuenda mazoezini au la hufanya na Fikra Fahamu.

Aina hii ya fikra au akili ya binadamu ndiyo ambayo hufundishwa vitu mbalimbali toka elimu ya kawaida toka mazingira anayoishi na elimu rasmi katika shule na vyuoni.

Fikra hizi hupokea elimu na kutunza kumbukumbu ambazo humuwezesha mtu kufanya mambo mbalimbali kama kuwasiliana,kuendesha gari,kutembea na kukumbuka majina na sura za watu au vitu.

2. Fikra za Kina (Subconscious Mind)

Fikra za kina ni mawazo yaliyolala na yanafundishwa kupitia na Fikra Fahamu. Fikra fahamu huwa kama mlango wa kupitisha elimu kuingia.Wakati mawazo ya kawaida yanapumzika mfano ukilala,mawazo ya kina huwa macho na hufanya kazi muda wote.Mambo yanayojirudia mara kwa mara huandikwa katika mawazo haya. Marudio ya mtendo yaleyale kwa muda mrefu hutunzwa katika Fikra ya kina.

Fikra za kina huhusika na matendo yote yasiyo ya kuchagua kama vile kupumua. Unaweza kupumua kwa kutumia mawazo ya kawaida(akili fahamu) mfano ukiwa unafanya mazoezi lakini baada ya hapo fikra za kina huendelea na kazi.

Fikra za kina zinahusika na tabia mbalimbali za binadamu na huongoza hisia ,ndio maana vitu kama woga,munkali,hasira au furaha haviwezi kuongozwa kirahisi na akili za kawaida. Pia katika Fikra za Kina ndiko ambako imani,hisia na kumbukumbu za muda mrefu hutunzwa.

Fikra hizi ni muhimu sana katika kuongoza hisia,matendo na matokeo ya binadamu yeyote na n muhimu kujua jinsi ya kuzitumia kiusahihi.

Namna ya Kutumia Fikra za Kina na Fikra Fahamu Kuleta Matokeo ya Malengo Yako.

Matokeo yoyote yanasababishwa na matendo na matendo ya binadamu yanaongozwa na hisia(sio akili ya ufahamu kama inavyodhaniwa). Mfano tamaa ya kuwa na mali inapelekea mtu kuanzisha biashara au kutafuta kazi yenye malipo makubwa. Tamaa ni hisia na haiongozi na akili ya ufahamu.

Lakini hisia pia zinaongozwa na Fikra za Kina ndani ya mwili wa binadamu. Fikra hizi ndizo zenye kuongoza hisia na mambo yasiyo ya hiari. Na nini kinaingiza habari katika Fikra za Kina?-Ni Fikra Fahamu au Fikra za Kawaida(Conscious Mind).

Mawazo ya kawaida yanatokana na elimu ambayo mtu anaipata toka katika vyanzo tofauti vitatu:

  • Mazingira yanayomzuguka,
  • Malezi toka kwa Wazazi na Walezi na Uzoefu kutokana na
  • Mambo yaliyomfika au kuona katika kipindi cha maisha yake.

Matokeo ni zao la mwisho la elimu,ufahamu,hisia na matendo yako

 Elimu–> Ufahamu–> Hisia –> Matendo ————->> MATOKEO
Yaani:

Elimu hujenga ufahamu katika akili ya kawaida,ufahamu kupitia mazoea na marudio hujenga hisia katika akili ya kina,na hisia katika akili ya kina hupelekea vitendo, na hatimaye vitendo huleta matokeo

Kwa mtazamo huu basi matokeo mazuri ya mipango na malengo yako hutokana na matendo ambayo husababishwa na hisia zinazongozwa na Fikra za Kina. Sababu kubwa za kutofanikiwa katika malengo yetu ni kunatokana na kuruka mojawapo ya hatua hizi tajwa hapa.

Ufahamu au elimu pekee haizai matokeo mazuri kama ambavyo inategemewa badala yake ni lazima kuhusisha fikra za kina ambazo zitajenga hisia kali ambazo husababisha vitendo na hatimaye huleta matokeo.

Hii inaelezea kwa nini wasomi wengi hawazalishi kama ambavyo inategemewa. Kinyume chake wale wenye ufahamu au elimu ya kawaida tu lakini wakafanya mambo kupitia hatua hizi hupata matokeo makubwa zaidi na kufanikiwa maishani.

Kushindwa Kunasababishwa na Watu Kutumia Mazoea Katika Kufanya Mambo

Mazoea hujenga tabia,na matendo yetu ya kila siku husababishwa kwa kiasi kikubwa na tabia zetu na sio elimu tulizopata mitaani au mashuleni. Na hapa ndio tunapata majibu ya swali la kuwa kwanini kuna utofauti mkubwa kati ya yale tuliyojifunza na kufahamu na yale tunayoyafanya?.

Tunajua kuwa kufanya mazoezi kila siku kwa dakika 15 tu kunaweza kukupunguzia uwezekano mkubwa wa kuugua,lakini hatufanyi mazoezi.

Tunafahamu kuwa kuvuta sigara kunaweza kukusababishia kansa na hata kifo, lakini watu wanaendelea kuvuta sigara. Hili ndio tatizo tunalozungumzia hapa. Utofauti kati ya ELIMU na MATENDO ya binadamu kunavyopelekea matokeo tusiyoyataka.  Matendo ni zao lakutumia Fikra za Kina na si elimu peke yake.

Kutumia Fikra Fahamu Kufundisha Fikra za Kina ili Kutoa Matokeo Sahihi

Fikra za Kina ambazo ndizo zinazoongoza matendo yetu zinaweza kufundishwa kupitia Fikra Fahamu. Fikra za Kina  zinafundishwa kwa marudio ya mambo unayotaka yatokee. Mfano unaweza ukaamua kuamka saa kumi na mbili kila siku asubuhi kwa msaada wa kengere ya saa yako au simu na ukafanya hivyo kwa kipindi cha mwezi mmoja. Baada ya hapo hata ukiacha kuweka kengere Fikra za Kina zitaendelea kukuamsha katika muda uleule.

Unaweza kufanya hivi kwa vitu vingine pia utakavyotaka. Mfano ukitaka kuanzisha biashara ambayo itatoa huduma kwa watu na kuwasaidia kumaliza matatizo yao basi panga mipango yako na kilasiku fikiria juu ya mpango wako.

Weka muda wa kufikiri juu ya mipango yako angalau dakika 10 kilasiku, kabla ya kuamka na kwenda kazini, mchana na usiku kabla hujalala. Hisia itajengeka kwa msaada wa fikra za kina na hatua zingine za uumbaji zitaendelea.

Unaweza ukaandika mawazo yako na malengo yako katika kitabu na uyasome kilasiku. Tengeneza kadi zenye malengo yako maishani na uziweke katika pochi yako na utembee nazo kila siku na kuzisoma, utajenga hisia na fikra za kina zitafanya hatua zilizobaki.

Vitendo vinavyoleta matokeo ya malengo yako vinatokana na hisia ndani yako.

Hebu Tufanye kwa Vitendo..

Sababu mojawapo watu hatufanikiwi ni kutochukua hatua za haraka. Chukua karatasi na kalamu sasa hivi na uandike malengo yako.

Kunja karatasi lenye malengo yako na weka katika pochi yako. Tembea nalo kila siku mpaka malengo yako yatakapotimia. Lisome angalau mara tatu kilasiku.

Fikiri juu ya malengo yako kwa dakika zisizopungua 10 kila siku na malengo yako yatafanikiwa. Kutumia fikra za kina kunafanya malengo yako yafikiwe kwa kujenga hisia kali ambazo zitapelekea kuchukua hatua kwa vitendo na mwishoni utapata matokeo uliyopanga.

Nawatakia mipango na matokeo mema!

Changia mawazo yako juu ya mada hii. Andika katika kisanduku cha majibu chini ya makala hii.

 

&

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment