Jamii Utamaduni

Mitindo Maridadi ya Nywele Asilia za Wanawake wa Kiafrika

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika_4

Mitindo ya nywele asilia kwa wanawake wa kiafrika ni mojawapo katika vitu vinavyojenga taswira na wasifu wake. Wanataaluma wa tabia za binadamu wanasema kuwa “Muonekano wako wa awali ndio mwonekano wako wa mwisho”. Maana yake kuwa jinsi ambavyo utaonekana mbele ya macho ya mtazamaji katika sekunde 30 za mwanzo unapotokea ndizo zinazokutambulisha wewe kuwa ni mtu wa aina gani hata mwisho.

Hitimisho ambalo mtazamaji atalifanya katika sekunde hizo 30 za mwanzo ndivyo atakazo baki nazo juu yako kuwa u mtu wa aina gani hata utakapoondoka machoni kwake.

Taswira ya mtu inajengwa kwa kiasi kikubwa na mavazi, uso na mtindo wa nywele. Pengine wanawake wa kisasa wanafahamu sana falasafa hii ndio maana wengi wao wanakazana sana na kupendezesha sehemu ya uso.

Leo nitaongelea kuhusu nywele hususani mitindo ya nywele asilia kwa wanawake wa kiafrika.

Kama nilivyosema awali kuwa mtizamo wako unachangia sana kuelezea kuwa wewe ni mtu wa aina gani.

Unaweza ukajua kama unajipenda au kujiheshimu kiasi gani kwa kuangalia tu staili ya nywele. Unaweza kujua mtu yupo katika kiwango gani cha kujitambua kama binadamu.

[ Soma Pia: Mitindo ya Kusuka Nywele za Asili: Jinsi ya Kuchagua Mtindo Bora ]

Kwa kutazama haraka tu utaweza kuona kuwa wanawake ambao wamefanikiwa sana kimaisha wanapenda mitindo rahisi ya nywele kuliko wale wenye maisha ya kati au ya chini kifedha.

Mfano nchini Tanzania,Mawaziri wengi wanawake husuka nywele zao mitindo rahisi kama vile “Twende Kilioni” au huchana tu nywele zao fupi au zikiwa ndefu huchana mtindo maarufu wa “Afro”.

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika_Dk-Fenela

Dk. Fenela Mukangara Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo wa Tanzania-Ni mfano mzuri katika kudumisha utamaduni wa nywele za kiafrika.

 

Nywele Asilia na Utu wa Mwafrika

Jamii yetu ya kiafrika imeathiriwa sana na tamaduni za kimagharibi. Wakoloni waliotutawala walisema kuwa mila zetu za kiafrika ni za kishenzi na zisizofaa. Wakaleta tamaduni na mila za kwao. Ni kweli tulikuwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na kwao lakini kuna baadhi ya vitu vilikuwa vizuri na vyenye kuwafaa waafrika.

Tulijengwa kuamini kila kitu cha kizungu ni kizuri kuliko cha kwetu. Tukabadili mitindo ya mavazi,majengo,jinsi ya kuabudu na hata mitindo ya nywele.

Athari hizi bado tunazo hadi leo, tumenaamini rangi nyeupe kama mzungu ni nzuri zaidi kuliko nyeusi, wanawake wa kiafrika wanakazana kubadilisha vipodozi vya kubadili rangi ya ngozi ili iwe nyeupe. Waulize wawe weupe kama nani? bila shaka majibu yatakuwa kama Mzungu au Mwarabu.

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika_mtindo-wa-kizungu

Mtindo wa Kuiga Nywele za Kizungu

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika_mtindo-wa-kiafrika

Mtindo Asilia wa Nywele za Kiafrika

Mitindo ya nywele hali kadhalika imabadilika sana,wanawake wa kiafrika leo wanabadili nywele zao kwa kutia madawa ya kuunguza nywele ili zifanane na wazungu. Kwani kitu kizuri kwetu bado ni kile cha kizungu.

Tumeacha mitindo yetu ya nywele yenye haiba ya pekee na tunang’ang’ania mitindo yao.

Tufahamu kuwa kila tunapojaribu kuwaiga wazungu ndivyo tunavyowaongeza thamani wao na kujishusha sisi wenyewe.

Ni muda muafaka sasa Waafrika tukarudi katika misingi yetu. Kuna mitindo mingi sana na maridadi ya nywele za kiafrika nitaitaja baadhi:

Twende Kilioni:

mitindo-ya-nywele-asilia-za-kiafrika-twende-kilioni

Nywele husukwa toka mbele ya uso na kuishia nyuma ya kisogo. Nywele fupi hadi kubwa zinaweza kusukwa kwa mtindo huu. Ni mtindo rahisi lakini maridadi sana.

Wanafunzi hupenda kusuka mtindo huu na unakubalika katika shule nyingi.

 

Kilimanjaro:

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika_kilimanjaro

Pengine asili ya msuko huu ni nchini Tanzania,kwani ndiko kuna mlima mrefu kuliko yote Afrika yaani Kilimanjaro.

Nywele husukwa toka pande zote za kichwa na kuishia utosini. Hapo mwishoni ncha zote za nywele hufungwa pamoja na kufanya kilele cha mlima wa nywele. Safi kweli kweli.

Mara nyingi mtindo huu unahitaji nywele nyingi na ndefu. Japo hata nywele fupi husukwa Kilimanjaro.

Rasta Asili:

mitindo-ya-nywele-asilia-za-kiafrika-rasta-asili

Nywele asili husokotwa badala ya kusukwa. Mtindo huu huwa unahitaji nywele kukaa kwa muda mrefu sana na unahitaji usafi wa hali ya juu,vinginevyo nywele zitatoa harufu.

 

Rasta za Bandia

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika-rasta-bandia

Nywele asili huongezewa nywele bandia. Lakini bado ni mtindo wa nywele ambao haumfanyi Mwafrika kuwa kama mzungu.

 

Afro

mitindo-ya-nywele-asilia-za -kiafrika-afro

Huu ni mtindo wa kuchana nywele bila kusuka. Nywele za saizi ya kati na ndefu zinafaa zaidi. Nywele zinachanwa kuelekea juu utosini na kutengeneza kitu mithili ya mwavuli wa nywele.

 

Ni rahisi kutengeneza na hauhitaji gharama kubwa. Mtindo huu unafaa kutengenezwa kwa ajili ya sherehe au mtoko wa jioni. Unapendeza sana. Binafsi naupenda kuliko mingine yote.

 

Afro Kifundo

Mtindo huu unafanana na Afro ya kawaida isipokuwa mtindo huu nywele hufungwa kwa uzi aidha juu ya utosi au kwa nyuma kisogoni. Mtindo huu unahitaji nywele ndefu.

 

Mabutu

mitindo-ya-nywele-asilia-za-kiafrika-mabutu

Ni mtindo rahisi wa kusuka nywele ambao nywele hufungwa mafungu mafungu. Ni mtindo unaotumika kwa muda kabla ya kusuka upya baada ya kufumua mtindo ungine.

 

Nywele za Uzi.

Ni adimu sana kuona aina hii ya ususi wa nywele siku hizi.

Nywele husokotwa kwa uzi kwa mafungu kama vile mabutu na kisha mikia ya mafungu hayo husukwa kwa namna tofauti.

 

Hitimisho

Kama tulivyoona ,hiyo ni baadhi tu ya mitindo mingi mbalimbali ambayo inawafaa na kuwapendezesha sana wanawake wa kiafrika na inayotunza mila na desturi zetu. Mitindo ambayo inatunza utu wa mwafrika.

 

Haya basi wanawake wakiafrika-turudi kwenye asili yetu ,turudie mtindo yetu ya nywele. Kwani ni mizuri na inathamani sana.

 

Je una mitindo mingine ya nywele unayoijua ambayo sijataja? Tafadhari ongeza kwenye kisanduku cha maoni hapa chini.

 

Toa maoni yako juu ya fikra hizi juu ya mitindo ya nywele na utu mwafrika.

 

Facebook Comments

Facebook comments

Leave a Comment

2 Comments

 • Umesahau mtindo mwngine wa nywele unaitwa ”mdomo wa kuku” huu ni mtindo wa kiasili kabisa. Pia kuna rasta unasokota kama Masai, yebo yebo na nyingine nyingi.

  • Asante Magreth kwa nyongeza. kama nilivyosema iko mitindo mingi sana.
   Nyongeza ya leo toka Magreth:
   1. Mdomo wa kuku: Kilimanjaro inayoishia upande mmoja wa kichwa
   2. Rasta Masai: Nywele zinasokotwa kama nyuzi nyembamba sana. Huwa zinachukua muda mwingi sana kukamilika na ni ghali kidogo
   3. Rasta za Yeboyebo: Nywele husukwa kwa kuongezea nywele bandia, ni mtindo maarufu na wanawake wengi husuka.